Skip to main content

Dkt. Mukwege ataka mahakama ya kimataifa DRC

Dkt. Mukwege ataka mahakama ya kimataifa DRC

Kikao cha 31 cha Baraza la Haki za Binadamu kikiendelea mjini Geneva Uswisi, bingwa wa matibabu dhidi ya wanawake waliokumbwa na ukatili wa kingono huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Daktari Denis Mukwege ameelezea wanachama wa baraza hilo wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo wakati nchi hiyo inaelekea uchaguzi mkuu mwisho wa mwaka huu.

Katika hotuba yake amewaomba wanachama hao watie saini ombi la kuondoa ukwepaji sheria kwa watekelezaji wa ukatili wa kingono nchini humo.

Daktari Mukwege ambaye amepewa tuzo mbalimbali za kimataifa kutokana na juhudi zake katika kutibu na kutetea wanawake walioathirika na matatizo ya kiafya baada ya kubakwa Mashariki mwa DRC, ametaka mahakama maalum ya kimataifa ianzishwe kwa ajili ya kufuatilia kesi za uhalifu wa kivita uliofanyika nchini DRC.

Kuhusu hali ya usalama iliyoko nchini humo akasisitiza

(sauti ya Dr Mukwege)

“ Ishara za onyo zimeangazia rangi ya hatari zaidi yaani nyekundu. Uwajibikaji wa kwanza ni kwa upande wa mamlaka za serikali na wadau wa kitaifa. Lakini hatuwezi kukubali machafuko yaanze tena nchini DRC baada ya miaka ya uwekezaji wa jamii ya kimataifa. Diplomasia ya kisiri ina kasoro zake. Hali iliyoko sasa hivi inaionyesha wazi. Kinga ni afadhali kuliko tiba.”