Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler alaani uwekwaji kizuizini wajumbe wa kamati ya usalama

Kobler alaani uwekwaji kizuizini wajumbe wa kamati ya usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL, Martin Kobler ameelezea kusikitishwa kwake kufuatia uwekwaji kizuizini kwa wajumbe watatu wa kamati ya muda ya  usalama TSC mjini Tripoli siku ya jumapili Machi sita.

Taarifa ya UNSMIL imemnukuu  Kobler akisema kuwa hatua hiyo ni kinyume na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa namba 2259 na inalenga kuizuia kamati ya usalama katika kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na usalama.

Amezikumbusha pande zote kuwa kamati hiyo ni chombo rasmi ambacho kinafanya kazi chini ya vigezo vya makubaliano ya kisiasa .

Mkuu huyo wa UNSMIL amezitaka pande husika na mamlaka kushirikiana kikamilifu na kuwezesha kazi ya TSC na kuhakikisha usalama wa wajumbe wake pamoja na uhuru wao wa kutoka sehemu moja hadi nyingine.