Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali tumeshuhudia ari ya kutekelezwa mkataba wa amani- Baraza

Mali tumeshuhudia ari ya kutekelezwa mkataba wa amani- Baraza

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamehitimisha ziara yao nchini Mali iliyowawezesha kuzuru maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ikiwemo Timbuktu na Mopti sambamba na kukutana na pande zote zilizotia saini makubaliano ya amani.

Mathalani wajumbe hao 15 walikutana na mashirika ya kiraia pamoja na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali na pande za upinzani ambapo mwishoni mwa ziara yao walizungumza na waandishi wa habari mjini Bamako.

Ziara yao ililenga kujionea hali halisi na kukutana uso kwa  uso na pande katika makubaliano ya amani ambapo kiongozi mwenza wa msafara Balozi Francois Delattre wa Ufaransa akasema..

(Sauti ya Balozi Delattre)

“Tumevutiwa sana, tumevutiwa na harakati na vile walivyo na ari ya kutekeleza makubaliano ya amani, na tumevutiwa pia na ubora na ubora wa hali ya juu wa wanawake na wanaume ambao wanaunda sehemu muhimu ya taifa hili la Mali ambalo tunalipenda sana.”

Hoja hiyo ikatiwa msisitizo na Rais wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Machi Balozi Ismael Gaspar Martins ambaye amesema tofauti na fikra za awali za kusuasua kwa utekelezaji wa mkataba, wakati huu wameshuhudia ari ya pande zote husika za kutaka kutekeleza mkataba ili kuleta hatimaye mabadiliko chanya sambamba na maendeleo yapatikane kaskazini mwa nchi yao.