Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia za kisasa mitandaoni zimeweka haki za mtoto hatarini- Mkutano

Teknolojia za kisasa mitandaoni zimeweka haki za mtoto hatarini- Mkutano

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mkutano wa siku moja kuhusu teknolojia za mawasiliano na utumikishaji wa kingono kwa watoto ambapo washiriki wameangazia changamoto katika ulinzi wa haki za mtoto katika zama za sasa za maendeleo ya teknolojia za mawasiliano. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Akifungua mkutano huo Rais wa Baraza hilo Choi Kyonglim amesema jambo la msingi ni kuibuka na njia zitakazowezesha mtoto kufurahia haki zake katika zama za sasa za mitandao badala ya usalama wake kuwa hatarini.

Naye mwenyekiti wa kamati ya mkataba wa haki za mtoto, Benyam Dawit Mezmur amesema mkataba huo haujagusia haki za mtoto katika teknolojia mpya za mawasiliano na intaneti akisema…

(Sauti ya Benyam)

Huu mkataba kama nyenzo zote za haki za binadamu, lazima uangaliwe kama nyenzo hai ambayo tafsiri yake inabadilika kadri muda unavyosonga. Hivyo sisi kama kamati tunawajibika na hili kwa dhati.”

Washiriki wametaka serikali kuweka sheria mahsusi ili kuondoa mianya inayosababisha wanaohusika na biashara ya ngono kwa watoto kupitia mitandao kukwepa mkono wa sheria.