Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za Binadamu lamulika mabadiliko ya tabianchi na haki ya afya

Baraza la Haki za Binadamu lamulika mabadiliko ya tabianchi na haki ya afya

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mjadala kuhusu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na kufurahia haki ya kuwa na afya bora kimwili na kiakili.

Mjadala huo umetokana na azimio la Baraza hilo namba 29 la mwaka 2015 kuhusu haki za binadamu na mabadiliko ya tabianchi, na unahusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa juhudi za nchi wanachama kutimiza haki ya kila mtu kufurahia kiwango bora zaidi cha afya kimwili na kiakili.

Katika hotuba yake kwa Baraza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dkt. Margaret Chan amesema mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa huathiri hewa wanayopumua watu, maji wanayokunywa, chakula wanachokila na uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.

WHO inakadiria kuwa kila mwaka, zaidi ya vifo milioni saba huenda vinasababishwa na uchafuzi wa hewa, na kwamba mabadiliko ya tabianchi yalisababisha makumi ya maelfu ya vifo kila mwaka kutokana na sababu zingine.”