Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Linalotia wasiwasi zaidi Yemen ni usalama wa raia- O’Brien

Linalotia wasiwasi zaidi Yemen ni usalama wa raia- O’Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, amekariri kauli yake kuwa pande zote kinzani katika mzozo wa Yemen zina wajibu wa kuchukua hatua zote zifaazo ili kuwalinda raia na miundombinu ya kiraia kila wakati, kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Bwana O’Brien amesema hayo akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limekutana leo kuhusu hali nchini Yemen. Afisa huyo wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa amesema, bila kuwepo muafaka wa kukomesha mzozo wa Yemen, hali ya usalama kote nchini humo inazorota kwa kasi kubwa.

“Mzozo nchini Yemen unaendelea kutokota tangu nilipolihutubia Baraza hili tarehe 16 Februari. Kwa kiwango kikubwa zaidi, linalotia wasiwasi zaidi sasa ni usalama wa raia, mamilioni yao wakikabiliwa na mashambulizi yasiyokoma na holela ya mabomu kutoka pande kinzani kila siku”.

Aidha, amelalama kuhusu vituo vya upekuzi vilivyoenea kila mahali nchini, na jinsi vinavyozuia utoaji huduma za kibinadamu, kupunguza kasi ya kusafirisha bidhaa na huduma muhimu, au hata kukwamisha kabisa usafiri.

“Licha ya ruhusa ya kusafiri, wakati mwingine malori hucheleweshwa kwa siku kadhaa au hata kwa wiki kadhaa. Vikwazo vya ukiritimba vilivyowekwa na mamlaka za Houthi, huchelewesha na kuzuia ufikishaji haraka misaada ya kibinadamu kwa wahitaji.”

Bwana O’Brien amesisitiza haja ya dharura ya Baraza la Usalama na jamii ya kimataifa kwa ujumla, kuweka shinikizo kwa pande kinzani katika mzozo wa Yemen kutimiza wajibu wao wa kuchukua hatua zaidi za kuwalinda raia, kuwezesha ufikiaji maeneo yote ya Yemen bila masharti, pamoja na kurejelea mazungumzo ya amani ili zifikie makubaliano ya kusitisha mapigano.