Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi kubwa ya tume ya Ulaya ni ishara njema kwa Global Fund

Ahadi kubwa ya tume ya Ulaya ni ishara njema kwa Global Fund

Tume ya Muungano wa Ulaya imetangaza ahadi ya Euro milioni 470 kwa mfuko wa kimataifa Global Fund kwa ajili ya kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria kwa miaka mitatu , kuanzia mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko la Euro milioni 100 au asilimia 27 ikilinganishwa  na mchango wao wa siku za nyuma.

Ahadi hiyo ni ishara ya uimara wa uongozi wa tume ya Muungano wa Ulaya katika afya ya kimataifa na ni ahadi ya kwanza ya awamu ya tano ya mfuko wa kimataifa , ufadhili utakaotumika kwa mzunguko wa mwaka 2017 hadi 2019.

Kwa mujibu wa Neven Mimica kamishina wa Muungano wa Ulaya kwa ushirikiano wa kimataifa na maendeleo, somo kutokana na mlipuko wa ebola Afrika Magharibi ni picha kamili kwamba kuna jhaja ya kuimarisha mifumo ya afya katika nchi zinazoendelea ili magonjwa ya mlipuko yaweze kudhibitiwa ipasavyo.

Euro hizo milioni 470 zitasaidia kutimiza sehemu ya lengo la Global Fund la kuokoa maisha ya watu milioni 8 ya kuepusha  maambukizi kwa watu milioni  300.

Kwa ujumla Muungano wa Ulaya unawakilisha asilimia 48 ya michango yote inayopokelewa na Global Fund.