Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa washikamana na Fiji baada ya kimbunga

Umoja wa Mataifa washikamana na Fiji baada ya kimbunga

Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Fiji, Osnat Lubrani, amesema leo kwamba Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kibinadamu kwa Pasifiki wanashikamana na serikali na raia wa Fiji katika kukabiliana na athari za kimbunga Winston kilichoathiri nchi hiyo tarehe 20 na 21 Februari.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kuratibu Maswala ya Kibinadamu (OCHA), imeeleza kwamba kimbunga hicho kilikuwa kibaya zaidi katika historia ya eneo la Pasifiki Kusini, kikishuhudia upepo wenye kasi ya kilomita zaidi ya 300 kwa saa, na kuua zaidi ya watu 21, huku watu wengine zaidi ya 8,000 wakiwa wamelazimika kuhama makwao na kutafuta hifadhi kwenye vituo vya dharura vilivyoandaliwa na serikali.

Bi Lubrini ameeleza pia kwamba Timu ya Umoja wa Mataifa inaendelea kujadiliana na serikali ya Fiji kufuatia ombi lake la kupata usaidizi wa kimataifa, ili kubuni na kuratibu misaada itakayopekwa.

Ameongeza kwamba picha zilizochukuliwa na serikali kutoka angani tayari zinaonyesha kiwango kikubwa cha uharibifu, ikiwa ni ishara ya kuhitaji muda mwingi kwa kukarabati nchi hii.