Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Uganda, mmoja afariki dunia, UM washutumu kuzuiwa mitandao ya kijamii

Uchaguzi Uganda, mmoja afariki dunia, UM washutumu kuzuiwa mitandao ya kijamii

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeshutumu serikali ya Uganda kwa kufunga mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi mkuu hii leo kwa madai ya kuimarisha usalama wa taifa huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki dunia kwenye ghasia zinazohusiana na uchaguzi.

Mwakilishi wa ofisi hiyo nchini Uganda Uchenna Emelonye amesema kitendo hicho cha kamisheni ya mawasiliano Uganda kinaingilia uhuru wa kujieleza akitaja mitandao husika kuwa ni pamoja na Whatapp ambayo ilifungwa tangu saa mbili asubuhi.

(Sauti ya Uchenna)

Tunaona suala hili kama kuingiliwa kw auhuru wa kujiuliza, hususan awakati wa uchaguzi hili linakuwa linaathiri mchakato wa demokrasia na uchaguzi wenyewe.  Kupata habari ni kitu muhimu wakati wa uchaguzi na suala kwamba mitandao ya kijamii imezuiwa na serikali ya Uganda siku ya uchaguzi, hili linaathiri uchaguzi huu nchini Uganda.”

Amesema tayari wamewasilisha malalamiko yao mbele ya mamlaka husika.

Halikadhalika, mwakilishi huyo wa ofisi ya haki za binadamu Uganda amezungumzia kasoro zilizojitokeza wakati wa upigaji kura ikiwemo kuchelewa kwa vifaa vya kupiga kura au kutowasili kabisa akisema hilo linaengua baadhi ya wapiga kura.

Bwana Emelonye amesema hoja  hiyo iliwasilishwa kwa tume ya uchaguzi ambayo ilieleza kuwa muda wa kupiga kura utafidiwa wakati huu ambapo ofisi hiyo inaendelea kufuatilia kwa karibu uchaguzi huo mkuu wa Rais na wabunge.