Afisa wa UM kuhusu amani na usalama azuru Burundi
Mwenyekiti wa Kitengo cha kuimarisha amani na usalama katika umoja wa mataifa yuko ziarani nchini Burundi. Bwana Jurg Lauber ambaye pia ni balozi wa Uswisi kwenye Umoja wa Mataifa amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza katika juhudi za kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo na kuinua uchumi wa nchi hiyo ulioathirika kutokana na ghasia zilizodumu kwa zaidi ya miezi 10.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na maswala ya haki za binaadamu Ivan Simonovic ameanza ziara nchini humo kutathimini hali ya haki za binadaamu na kuandaa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon baadaye mwezi huu.Kutoka Bujumbura, Mwandishi wetu Ramadhani KIBUGA anasimulia zaidi.
(TAARIFA YA KIBUGA)
Mwenyejiti wa Kitengo cha kuimarisha amani na usalama katika Umoja wa Mataifa anayehusika na Burundi ambaye pia ni Balozi wa Uswisi kwenye shirika hilo Jurg Lauber amesema shabaha ya ziara yake ni kutathimi hali halisi ya usalama Burundi na njia za kukwamua mgogoro lakini pia kuinua uchumi wa taifa kama alivyosema muda mfupi baada ya kupokelewa kwa mazungumzo na Rais wa burundi Pierre Nkurunziza.
(SAUTI YA JURG LAUBER)
“Tumezungumzia kuhusu hali ya usalama nchini, kuhusu mazingira ya mazungumzo ya kisiasa ndani ya nchi na kuhusu hasa hali ya kiuchumi. Nimetilia hasa mkazo kuhusu hali ya uchumi kwenye mazungumzo yangu na rais , kama mnavojuwa uchumi umeathirika zaidi kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoisibu Burundi tangu mwaka jana na ambao unaendelea na tumezungumzia uwezekano wa kupanua ushirikiano zaidi kati ya burundi na Umoja wa Mataifa na kitengo hiki pamoja na zingine idara za Umoja wa mataifa ili kuinua hali ya uchumi wa nchi “
Kwa mujibu wa Naibu msemaji wa Rais wa Burundi Claude Karegwa, Rais Nkurunziza amesifu mchango wa Umoja wa Mataifa .
(SAUTI YA KAREGWA)
“Rais amempongeza kuhusu juhuzi zinazofanywa na Umoja wa mataifa kusaidia Burundi na kumuhakikishia kuwa serikali ya Burundi kama inavoombwa itafanya kila iwezalo ili kuimarisha amani na usalama nchini pamoja na kutunisha uchumi wa taifa ili kustaawisha wananchi. Rais pia ameutaka Umoja wa Mataifa wasaidie kutoa msukumo ili Tume ya Ukweli na Mariadhiano ifanye kazi maana shughuli za tume hiyo ndio itakamilisha mpango wa amani."