Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MONUSCO aanza ziara mashariki mwa DRC

Mkuu wa MONUSCO aanza ziara mashariki mwa DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ujumbe wa umoja huo nchini humo, MONUSCO, Maman Sambo Sidikou leo ameanza ziara ya siku nne kwenye jimbo la Kivu Kaskazini.

Lengo la ziara hiyo inayomjumuisha pia mwakilishi wa kanisa katoliki nchini humo Luis Mariano Montemayor ni kuonyesha mshikamano na kuwatia moyo wananchi wa maeneo ya Goma na Kitchanga kufuatia madhila yaliyowakumba ikiwemo visa vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto na mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami.

Charles Bambara, Mkurugenzi wa mawasiliano wa Monusco akihojiwa na Idhaa hii amesema ziara hiyo ni nyongeza ya kando ya juhudi za kijeshi za kuleta amani kwenye eneo hilo na akaeleza mipango ya baadaye ya kujumuisha viongozi wa imani nyingine za dini..

(Sauti ya Bambara)

“Mwakilishi maalum tayari anawasiliana na viongozi wa jamii ya kiislamu hapa DR Congo, alikutana nao hapa Kinshasa na amepanga kukutana pia na viongozi wa imani nyingine za dini na kuna mipango mingine, huu ni mwanzo tu.”