Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiongozi wa OCHA aangazia hali ya kibinadamu Eritrea na Ethiopia

Kiongozi wa OCHA aangazia hali ya kibinadamu Eritrea na Ethiopia

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, Kyung-wha Kang, amehitimisha ziara ya siku tatu nchini Eritrea akisihi jumuiya ya kimataifa kuongeza usaidizi wake kwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Bi Kang amekutana na viongozi wa serikali na kutembelea vituo vya afya vinavyoongozwa na serikali kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, akishuhudia hatua zilizopigwa na serikali katika kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Halikadhalika Bi Kang amezungumza na waandishi wa habari Addis Ababa nchini Ethiopia kuhusu athari za ukame uliosababishwa na El-nino nchini humo, ambazo kwa mujibu wake ukali wake unalingana na ule wa El-nino wa mwaka 1997.

Amesema zaidi ya watu milioni 10 wanakadiriwa kuhitaji msaada wa kibinadamu nchini Ethiopia, idadi hiyo ikiweza kuongezeka iwapo hatua hazitachukuliwa ili kusaidia sekta ya kilimo na mifugo.