Burundi yakataa mazungumzo ya kisiasa, UM waiomba ishiriki

Burundi yakataa mazungumzo ya kisiasa, UM waiomba ishiriki

Umoja wa Mataifa unaiomba serikali ya Burundi ishiriki mazungumzo ya kisiasa, ukielezea kuendelea kuwa na wasiwasi kuhusu mauaji yanayozidi nchini humo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo akijibu swali wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari leo mjini New York Marekani alipoulizwa msimamo wa Umoja huo kuhusu tangazo la Burundi la kukataa kushiriki mazungumzo ya amani huko Arusha, Tanzania.

(Sauti ya Bwana Dujarric)

“ Tunaiomba serikali ya Burundi kushiriki mazungumzo ya kisiasa. Ni wazi kwamba mazungumzo yatakayosongesha nchi mbele yanapaswa kujumuisha pande zote ikiwemo serikali, Nadhani pia ghasia tunayoshuhudia italazimisha pande zote kuongeza jitihada zao maradufu katika mazungumzo ya kisiasa.”

Awali serikali ya Burundi ilielezea haiwezi kushiriki mazungumzo yaliyokuwa yameitishwa hii leo mjini Arusha Tanzania, kwa madai kuwa haiko tayari kuzungumza na watu wanaoshukiwa kushiriki jaribio la mapinduzi.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Katibu wa kudumu katika Wizara ya mambo ya nje ya Burundi Balozi Joseph Bangurambona amesema serikali haitashiriki mazungumzo leo wala tarehe nyingine.

(Sauti ya Joseph Bangurambona)

“ Serikali ya Burundi haijaelewana na upatanishi juu ya tarehe mpya ya mazungumzo, inabidi kwanza kuelewana kuhusu baadhi ya maswala kabla ya kuingia kwenye mazungumzo. Kwa hiyo serikali iko wazi haiwezi kuketi mezani na watu waliochukua njia ya mapambano. Na kama Umoja wa mataifa ulivyobainisha mazungumzo yawepo lakini wasiingie watu wenye mpango wa vita. ”