Ban alaani jaribio la nyuklia DPRK, asema latia hofu kubwa

Ban alaani jaribio la nyuklia DPRK, asema latia hofu kubwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani jaribio la nyuklia chini ya ardhi lililotangazwa kufanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, leo Januari 6, akisema linatia hofu kubwa. Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Akiongea mbele ya waandishi wa habari jijini New York Jumatano asubuhi, Ban amesema jaribio hilo la nyuklia linakiuka maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama, licha ya wito wa pamoja wa jamii ya kimataifa wa kukomesha vitendo kama hivyo.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa jaribio hilo linakiuka kwa kiasi kikubwa kanuni ya kimataifa dhidi ya majaribio ya nyuklia.

Ban amelaani kitendo hicho, akisema kuwa kinavuruga usalama wa kikanda na juhudi za kimataifa za kupinga uenezaji wa silaha za nyuklia.

“Naitaka DPRK ikome vitendo vyovyote zaidi vya nyuklia, na itimize wajibu wake kuhusu uondoaji wa silaha za nyuklia unaoweza kuthibitishwa. Tunafuatilia na kutathmini hali kwa uratibu wa karibu wa mashirika husika ya kimataifa, yakiwemo Shirika la Kupinga Majaribio ya Nyuklia, CTBTO na wadau wengine.”