Skip to main content

Tumenasa mitetemo isiyo ya kawaida huko DPRK: CTBTO

Tumenasa mitetemo isiyo ya kawaida huko DPRK: CTBTO

Shirika la Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya silaha za Nyuklia, CTBTO, limesema kuwa vituo vyake vya ufuatiliaji vilinasa mitetemo isiyo ya kawaida kwenye eneo la nchi hiyo majira ya usiku. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katibu Mtendaji wa CTBTO Lassina Zerbo amesema makadirio ya awali yanaonyesha kufanyika katika eneo la nyuklia la DPRK wakati huu ambapo nchi hiyo tayari imedai kufanya jaribio la nyuklia ambalo ni la nne tangu mwaka 2006.

Bwana Zerbo amesema iwapo itathibitishwa ni jaribio la nyuklia, kitendo hicho kitakuwa ni ukiukwaji wa makubaliano ya kimataifa yaliyoridhiwa na nchi 183 tangu mwaka 1996 na zaidi ya hapo ni tishio la amani na usalama duniani.

Ameisihi DPRK kujizuia na majaribio zaidi ya nyuklia na badala yake iungane na mataifa 183 yaliyotia saini mkataba wa kupinga majaribio ya silaha za nyuklia, CTBT.

Amesema wakati jamii ya kimatifa inaadhimisha miaka 20 tangu kuanza kutiwa saini kwa mkataba huo ni vyema udhibiti wa matumizi hayo ukakisiwa katika mkataba wenye nguvu kisheria.

Mtendaji huyo wa CTBTO amesema tukio la leo ni wito wa mwisho kwa jamii ya kimataifa kuharamisha majaribio yote ya nyuklia kwa kuanza matumizi ya mkataba huo.