Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na asasi ya Uingereza zashirikiana kuimarisha huduma za maji na kujisafi Syria

UNICEF na asasi ya Uingereza zashirikiana kuimarisha huduma za maji na kujisafi Syria

Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF, linashirikiana na Shirika la kutoa misaada la Uingereza, UK AID kuimarisha huduma za maji safi na kujisafi katika shule za Syria, ili kuhakikisha kuwa kila mtoto nchini humo anafurahia haki yake ya kuwa na mazingira ya kusoma yenye afya.

Mashirika hayo yameanza ushirikiano wao kwa kukarabati vyoo, sehemu za kunawa mikono na mabwawa ya maji katika shule 80 kwenye mikoa miwili ya Tartous na Lattakia, ili kuwezesha watoto zaidi ya 65,000 kupata huduma za maji safi na kujisafi.

Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 95,000, wengi wao wakiwa wamefurushwa na machafuko kutoka maeneo ya Aleppo, Idleb, Homs na Damascus vijijini sasa wanaishi Tartous na Lattakia, ambako kuna uhaba wa huduma za maji na vifaa vya kujisafi.