Mazungumzo kuhusu Burundi yaanza Kampala, UM wahimiza mashauriano

28 Disemba 2015

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi, Jamal Ben Omar, ametoa wito kwa pande kinzani nchini Burundi zitafute suluhu la makubaliano kwa mzozo unaoikabili nchi yao. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya John Kibego)

Bwana Ben Omar amesema hayo wakati wa mazungumzo ya amani yaliyoanza leo mjini Kampala, Uganda, yakiongozwa na mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Bwana Ben Omar amesema, kama Baraza la Usalama liliposisitiza katika taarifa yake ya hivi karibuni zaidi kuhusu Burundi, mazungumzo hayo ni lazima yafanyike katika mazingira stahiki ya usalama, na kwamba kuna haja ya kuwezesha ushiriki na uwakilishi kamilifu wa wadau wote wa Burundi, na maoni yao kuhusu masuala tatanishi.

(Sauti ya Bwana Ben Omar)

“Burundi imepitia wakati mgumu zamani, na ina historia ndefu ya mashauriano. Kuna mafunzo yanayoweza kutokana na uzoefu huu wa zamani. Warundi ndio watakaoishi na matokeo ya maamuzi watakayofanya. Wana wajibu wa msingi wa kutafuta njia ya kwenda mbele, kwa mustakhbali wa nchi yao”

Naye Rais Museveni kama mpatanishi wa mazungumzo hayo, akafunguka..

(Sauti ya Rais Museveni)

“Natoa wito kwenu pande mbili. Kaeni chini na mpate suluhu la kisiasa, ili muwaokoe watu wetu kutokana na mateso wanayopitia sasa”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter