Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakaribisha kuhitimishwa kwa kazi ya ICTR, lataka ICTY ifuate hima

Baraza la Usalama lakaribisha kuhitimishwa kwa kazi ya ICTR, lataka ICTY ifuate hima

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limepitisha azimio linalokaribisha kuhitimishwa kwa kazi ya kisheria ya Mahakama ya Kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari Rwanda, ICTR, kufuatia mahakama hiyo kutoa hukumu yake ya mwisho mnamo Disemba 14, mwaka huu, mahakama hiyo inapokaribia kufungwa mwishoni mwa mwaka huu.

Wakikaribisha kuhitimishwa kwa kazi ya ICTR, wajumbe wa Baraza la Usalama pia wameongeza muda wa majaji wa mahakama ya kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari Yugoslavia, ICTY, na kuitaka mahakama hiyo iongeze kasi ya utendaji kazi wake, ili ikamilishe majukumu yake haraka iwezekanavyo, na kutoa ripoti kwa baraza hilo mwishoni mwa mwezi Juni 2016.

Aidha, Baraza hilo limekaribisha kukamatwa kwa Ladislas Ntangazwa mnamo Disemba nane nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, lakini likaeleza kusikitishwa kwamba bado kuna washukiwa wengi wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda wanaoendelea kukwepa mkono wa sheria.

Baadaye Baraza la Usalama limekuwa na kikao kuhusu hali nchini Yemen, ambako Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

(Sauti ya Zeid)

“Zaidi ya hayo, ofisi yangu imegundua kuwa bado kuna kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi, uharibifu wa mali na miundombinu ya kiraia, na uzuiliaji wa raia unaotendwa na pande zote katika mzozo”