Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaposhughulikia majanga tusisahau ajenda muhimu za dunia: Ban

Tunaposhughulikia majanga tusisahau ajenda muhimu za dunia: Ban

Kadri tunavyokabiliana na majanga ya Ukraine, Syria, Sudan Kusini na ukatili huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hatupaswi kusahau mambo muhimu ambayo yanaweza kuonekana hayana uharaka lakini ni vitisho vya muda mrefu iwapo yatapuuzwa.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika mhadhara aliotoa leo kwenye Chuo Kikuu cha Charles huko Prague, Jamhuri ya Czech ambako ametuzwa medali ya dhahabu kwa mchango wake wa kusaka amani.

Ban amesema dunia sasa iko njiapanda kwani kuna mizozo hiyo inatokea huku kukiwa na mambo matatu kwenye ajenda ya itakayoonyesha mwelekeo wa dunia, akisema mwaka 2015 ni mwaka wa dunia kufanya uamuzi.

Amesema Mosi ni malengo ya maendeleo ya Milenia yanayofikia ukomo mwakani ambapo umaskini umepunguzwa kwa asilimia 50 lakini bado safari ni ndefu. Suala lingine ni maandalizi ya ajenda endelevu baada ya 2015 akisema lazima iwe jumuishi ikizingatia uendelevu wa kiuchumi, kijamii na mazingira na mwisho akasema ni mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Ban amesema changamoto hizo ni kubwa na zinataka umoja na ndio maana anahusisha wahusika stahili wa kuleta mabadiliko duniani akitaja wanawake na vijana.

“ Ndani ya Umoja wa Mataifa wenyewe, nimeteua idadi inayovunja rekodi ya wanawake kushika nyadhifa za juu. Sikujaza nafasi hizo kwa kuwa ni wanawake tu, bali niliangalia mwombaji nafasi ya kazi na ukiondoa ubaguzi, mwomba ajira bora zaidi na mwenye sifa mara nyingi ni mwanamke.”