Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kuhusu ukatili wa kingono CAR

Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kuhusu ukatili wa kingono CAR

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameahidi kupitia mara moja mapendekezo yaliyotolewa na jopo huru kuhusu ukatili wa kingono unaodaiwa kufanywa na wanajeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo akizungumza leo na waandishi wa habari, siku ambayo ripoti hiyo imechapishwa, akiongeza kwamba wanajeshi hao hawakuwa chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo amesema ripoti imeonyesha kwamba wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa walitumia vibaya mamlaka yao, wengine wakiwa wamekosa ufanisi katika kazi zao.

(Sauti ya Bwana Dujarric)

«  Ripoti imeonyesha kwamba Umoja wa Mataifa umeshindwa kuchukua ipasavyo pindi ulipopokea taarifa ya uhalifu dhidi ya watoto walio hatarini zaidi. Katibu Mkuu amesikitishwa kwamba watoto hao wamelaghaiwa na watu wale wale waliokuwa na wajibu wa kuwalinda. Licha ya kwamba wanajeshi waliotekeleza ukatili huo hawakuwa chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa, ripoti inaonyesha kwamba Umoja wa Mataifa uliogundua uhalifu huo haukuchukua hatua dhidi ya tukio hilo na kazi na umakini uliotakiwa. »

Jopo hilo huru lililoongozwa na jaji Marie Deschamps kutoka Canada, liliteuliwa na Katibu Mkuu Ban mwezi Juni mwaka huu kwa lengo la kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono na ukatili dhidi ya watoto uliodaiwa kufanywa na wanajeshi wasio chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa.