Skip to main content

Jopo huru la wataalamu kwenda Burundi kufanya uchunguzi: Azimio

Jopo huru la wataalamu kwenda Burundi kufanya uchunguzi: Azimio

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kumtaka kamishna mkuu kuunda jopo la wataalamu huru kwenda Burundi haraka ambapo pamoja na mambo mengine litachunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.

Azimio hilo limepitishwa leo mwishoni mwa kikao maalum cha Baraza hilo kuhusu Burundi kilichofanyika huko Geneva, Uswisi ambapo limesema uchunguzi huo wa jopo hilo huru unalenga kuepusha kuzorota zaidi kwa hali ya haki za binadamu nchini humo.

Halikadhalika jopo hilo litapendekeza jinsi ya kuimarisha hali ya haki za binadamu na usaidizi wa kuwezesha Burundi kutekeleza mkataba wa Arusha.

Wajumbe wa baraza hilo wameitaka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kuwezesha jopo hilo kutekeleza wajibu wake.