Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji haramu wa binadamu ni utumwa, lazima ukomeshwe- Eliasson

Usafirishaji haramu wa binadamu ni utumwa, lazima ukomeshwe- Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, ameutaja usafirishaji haramu wa binadamu kama utumwa wa kisasa, na kwamba sio tu uovu wa kale.

Bwana Eliasson amesema hayo akihutubia Baraza la Usalama, ambalo limekutana kujadili kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu katika hali za migogoro.

Amesema hata wakati huu, mwaka 2015, bado mamilioni ya watu wanaishi kama watumwa, katika mazingira kama ya utumwa. Ameongeza kwamba wengi watu wanaosafirishwa haramu ni wanawake na watoto wanaodanganywa au kutekwa na kuingizwa katika maisha ya mateso, unyanyasaji, na utumwa.

“Vitendo hivi vya kinyama vimefanywa kuwa sekta ya biashara kimataifa, na ni lazima vikomeshwe. Nimeguswa kwamba nchi wanachama ziliahidi, kama sehemu ya malengo namba tano, nane na kumi na sita ya ajenda ya 2030, kuchukua hatua dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu.”

Aidha, Bwana Eliasson amesema kuwa duniani sasa kuna idadi kubwa zaidi ya watu waliolazimika kuhama makwao kuliko wakati mwingine wowote tangu vita vikuu vya pili vya dunia, na kwamba watu hawa hujikuta katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ukiwemo usafirishaji haramu.

“Wanauzwa, wanasafirishwa kwa utumwa wa kingono, biashara ya ngono, kuingizwa katika familia kiharamu, katika uhalifu au kama watoto wanajeshi. Wahanga kwa wingi ni wanawake na wasichana, lakini pia wavulana na wanaume. Maelfu ya wanaume na wavulana wamelasajiliwa kwa lazima na LRA na vikundi vingine vyenye silaha.”