Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto ndio wahanga zaidi wa magonjwa yaambukizwao kupitia chakula.

Watoto ndio wahanga zaidi wa magonjwa yaambukizwao kupitia chakula.

Ripoti ya kwanza kabisa ya shirika la afya duniani, WHO kuhusu maradhi yaambukizwao kupitia chakula imeonyesha kuwa watoto ndio waathirika zaidi na mifumo dhaifu ya usalama wa chakula ikitajwa kuwa moja ya sababu. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Ikiwa ni makadirio ya kwanza kabisa kufanyika duniani kote, ripoti hiyo inasema asilimia 30 ya vifo vitokanavyo na maambukizi kwenye chakula vinakumba zaidi watoto ikiwa ni watoto Laki Moja na Elfu Ishirini na Tano kila mwaka.

Bara la Afrika na nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia ndio zinabeba idadi kubwa zaidi ya vifo ambapo ripoti inasema sababu ni maambukizi yatokanayo na kula vyakula vyenye bakteria hatarishi, virusi na kemikali zenye sumu.

Dokta Kazuaki Miyagishima, ni Mkurugenzi wa Idara ya usalama wa chakula ndani ya WHO.

(Sauti ya dkt Kazuaki)

"Siku hizi jambo muhimu ni kwamba biashara ya chakula imekuwa kutokana na utandawazi na hivyo iwapo kuna nchi ambayo mfumo wake wa usalama wa chakula ni dhaifu, na nchi hiyo inauza nje chakula hicho kwa nchi nyingine, basi nchi hiyo itakuwa  chanzo cha udhaifu kwenye mfumo wa uzalishaji wa chakula. Na ndiyo maana WHO inataka kusaidia kuimarisha mifumo ya usalama wa chakula kwenye nchi ambako ni dhaifu na hii itaimarisha usalama wa chakula duniani.”