Skip to main content

Siku ya utumwa duniani yamulika mateso ya watumwa milioni 21 wa kisasa

Siku ya utumwa duniani yamulika mateso ya watumwa milioni 21 wa kisasa

Bado inakadiriwa kwamba watu wapatao milioni 21 duniani kote ni watumwa wa kisasa amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwenye ujumbe wake, leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza utumwa, akiongeza kwamba watu zaidi ya milioni 60 waliolazimika kuhama makwao wako hatarini kutumikishwa. Taarifa zaidi na Joseph Msami.

(Taarifa ya Msami)

Bwana Ban amesema  utumwa wa kisasa unajitokeza kwa njia mbalimbali ikiwemo utumikishwaji wa watoto kwenye viwanda, kilimo au majumbani, wafanyakazi wanaodaiwa madeni na waajiri wao, ama watumishi wa biashara ya ngono.

Ili kutokomeza utumwa, Katibu Mkuu amesihi nchi wanachama, kampuni na wadau wengine kufadhili mfuko wa Umoja wa Mataifa kuhusu aina za kisasa za utumwa ili kusaidia wahanga wa uhalifu huo na kuwawezesha kuanza upya maisha ya kawaida.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kazi ILO, Guy Rider amezisihi serikali kuridhia mkataba wa ILO kuhusu utumikishwaji.

(Sauti ya Ryder)

"Leo tunaakisi kitu gani twaweza kuboresha pamoja, ili kufanikisha lengo la pamoja la kukomesha utumwa wa kisasa. Miongoni mwa makusudio ya lengo  namba nane la melengo endelevu SDG linalotaka kukuza kazi bora, ujumuishwaji na ukuaji endelevu,  ni hatua za haraka na fanisi za kukomesha utumikishwaji kazini, utumwa wa kisasa na usafirishaji haramu wa binadamu.’’