Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila fursa kwa vijana, nchi za Sahel kuzidi kukumbwa na ugaidi: Mtalaam wa UN

Bila fursa kwa vijana, nchi za Sahel kuzidi kukumbwa na ugaidi: Mtalaam wa UN

Baraza la Usalama leo limekuwa na mjadala maalum kuhusu amani na usalama kwenye ukanda wa Sahel, ambapo Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sahel, Hiroute Guebre Sellasie ameliomba baraza hilo kuuangazia zaidi ukanda huo unaokumbwa na vitisho vya ugaidi, umasikini na mabadiliko ya tabianchi. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Kwenye hotuba yake mbele ya Baraza la Usalama Bi Guebre Selassie amesema nchi za Sahel ni wahanga wa matatizo yanayovuka mipaka yao na kuzidi uwezo wao wa kukabiliana nayo.

Ameongeza kwamba moja ya misingi ya changamoto hizo ni ukosefu wa matumaini kwa vijana wa eneo hilo, huku asilimia 56 tu ya watoto wakiwa wameandikishwa shuleni.

(Sauti ya Bi Guebre Selassie)

"Iwapo hakuna kitu kitakachofanyika ili kuimairsha upatikanaji wa huduma ya elimu, upatikanaji wa ajira, fursa kwa vijana na kujumuisha jamii, niko na wasiwasi kwamba Sahel itakuwa kitovu cha uhamiaji wa wengi, ajira na mafunzo kwa vikundi vya kigaidi na hilo litakuwa na matokeo hatari sana kwa usalama na amani ya kimataifa."

Akisisitiza kwamba biashara ya madawa ya kulevya inachangia pia katika kufadhili ugaidi, Bi Guebre Selassie ametoa wito kwa Baraza la usalama liongeze juhudi za kufuatilia vikundi hivyo vya kigaidi na vyanzo vyao vya ufadhili akiiomba pia jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa ukanda huo.