Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Yemen, 26% ya maduka yamefungwa : UNDP

Nchini Yemen, 26% ya maduka yamefungwa : UNDP

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP limezindua leo matokeo ya utafiti kuhusu athari za vita katika sekta ya biashara nchini Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo, asilimia 26 ya biashara zimefungwa nchini humo tangu mwezi Machi mwaka huu kutokana na machafuko, sababu ya kwanza ikiwa ni kubomolewa kwa maduka yao.

Aidha ripoti imeeleza kwamba wanawake wafanyabiashara wameathirika zaidi na mzozo huo, karibu nusu ya maduka yaliyomilikiwa na wanawake yakiwa yamefungwa.

UNDP imeeleza pia kwamba Yemen ikitegemea vyakula vinavyoagizwa kutoka nje kwa asilimia 90, vizuizi dhidi ya bidhaa zinazotoka nje vinaathiri sana wafanyabiashara ambao wanahaha kujaza maduka yao. Ukosefu wa huduma za benki na ufadhili pia hukumba wafanyabiashara hao.

Kwa mantiki hiyo UNDP imeshauri wadau kusaidia sekta ya biashara Yemen ili ijengewe uwezo wa kustahamili mizozo, na kulenga zaidi vijana na wanawake katika misaada yao.