Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP21 izingatie matumizi ya nishati ya nyuklia:IAEA

COP21 izingatie matumizi ya nishati ya nyuklia:IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA Yukiya Amano amesema matumizi ya nishati ya nyuklia yapatiwe msisitizo wakati wa mkutano wa 21 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP21 utakaonza wiki mbili zijazo huko Paris Ufaransa.

Akiwasilisha ripoti ya mwaka ya IAEA mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano Bwana Amano amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa nchi nyingi duniani hivi sasa zinatama nishati ya nyuklia kama mkombozi  katika kupata nishati ya uhakika na wakati huo huo kupunguza gesi chafuzi.

Kwa hiyo amesema..

“Nishati ya nyuklia ina athari ndogo sana kwa mazingira na inawezesha kuepuka utoaji wa gesi chafuzi. Naamini uzingatiaji wa uhakika unapaswa kuzingatiwa wakati wa mazungumzo kuhusu kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi chini ya mfumo wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa mujibu wa Amano, kwa sasa kuna vinu 441 vya nishati ya nyuklia katika nchi 30 duniani ambapo kwa pamoja inachangia asilimia 11 ya nishati ya umeme ulimwenguni kote.

IAEA imesema barani ASIA kuna vinu 65 vya nishati ya nyuklia vinajengwa hivi sasa ambapo inasaidia nchi kuhakikisha vinakuwa salama na endelevu.