Skip to main content

Kamisheni ya amani kupokea ripoti kuhusu Burundi

Kamisheni ya amani kupokea ripoti kuhusu Burundi

Mwenyekiti wa mfumo wa kushughulikia amani Burundi ulio chini ya Kamisheni ya Ujenzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, Jurg Lauber leo Jumatano anatarajiwa kuhutubia kamisheni hiyo kuhusu tathmini ya ziara yake aliyofanya nchini humo hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Lauber mwishoni mwa ziara yake alielezea  wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa chuki miongoni mwa jamii unaoshamiri na ambao amesema unaweza kuchochea chuki zaidi.

Katika ziara hiyo Bwana Lauber amekutana na rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, viongozi wa serikali, wawakilishi wa jamii na wa mashirika ya kikanda na ya Umoja wa Mataifa wakijadiliana kuhusu hali ya usalama, utaratibu wa mazungumzo, na athari za kiuchumi za mzozo huo.

Bwana Lauber ameiomba serikali na vyama vya upinzani vishiriki mazungumzo shirikishi ili kurejesha uaminifu kwa raia wa Burundi, akisema bado kuna fursa ya kutatua mzozo huo kwa njia ya amani licha ya hali ya kisiasa kuhitaji hatua za dharura.

Ziara hiyo pia ilimpeleka Uganda na Tanzania ambako amezungumza na viongozi waandamizi kuhusu suala hilo.