Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wasigeuzwe kuwa visingizio vya mashambulizi ya Paris- UNHCR

Wakimbizi wasigeuzwe kuwa visingizio vya mashambulizi ya Paris- UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limeeleza kushtushwa na kusikitishwa na mashambulizi ya Paris na mauaji ya watu wengi wasio na hatia, lakini likatoa wito wakimbizi wasisingiziwe kuwa sababu ya mashambulizi hayo.

Katika taarifa, UNHCR imesema wengi wa watu wanaokimbilia Ulaya wanatoroka mateso au athari za mzozo unaotishia maisha yao, na kwamba hawana njia nyingine ya kuingia Ulaya, huku hali mbaya katika nchi wanakowasili kwanza wakisaka hifadhi zikiwalazimu kujaribu kwenda Ulaya.

Aidha, UNHCR imesema wengi wa wakimbizi hao wanatoroka itikadi kali na ugaidi unaoenezwa na watu wale wale waliohusika katika mashambulizi ya Paris. Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR Geneva

“Tunasikitishwa mno na lugha inayowabagua wakimbizi kama kundi la watu. Hii ni hatari, kwani itachangia chuki za kibaguzi na uoga. Matatizo ya kiusalama yanayoikabili Ulaya ni tata. Wakimbizi wasigeuzwe kuwa visingizio, na wasifanywe kuwa wahanga wa daraja ya pili ya matukio haya ambayo ni janga kubwa.”

Wakati huo huo, UNHCR imeeleza kusikitishwa na habari ambazo hazijathibitishwa kuwa mmoja wa washambuliaji wa Parish huenda aliingia Ulaya katika wimbi la sasa la wakimbizi.