Skip to main content

Watu 26 wakadiriwa kufariki dunia Yemen kutokana na vimbunga

Watu 26 wakadiriwa kufariki dunia Yemen kutokana na vimbunga

Inakadiriwa kuwa watu 26 wamefariki dunia kutokana na vimbunga vilivyoikumba Yemen hivi karibuni, 18 kati yao kwenye kisiwa cha Socotra, kwa mujibu wa mamlaka nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na leo na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imesema kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanajikita katika kutoa misaada ya kibinadamu ili kupunguza maafa zaidi.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na wadau wake wanasambaza biskuti za kuongeza nguvu kwa watu 25,000, huku lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likisambaza vifaa vya nyumbani na mahema kwa watu wapatao 2,700 kwenye kata ya Shabwah, na kwa watu 2,500 kwenye kata ya Hadramaut.

Taarifa ya OCHA imeongeza kuwa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM linaendelea kutoa misaada ya maji safi kata za Shabwah na Abyan , ingawa uhaba wa mafuta umepunguza idadi ya watu wanaofikiwa.

Wadau wa afya katika Umoja wa Mataifa wanafuatilia uwezekano wa milipuko ya magonjwa, huku Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF likipanga kutoa vifaa vya kujisafi Hadramaut na Shabwah.