Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu ya simu kuwezesha mtu kuchangia mlo wake na mtoto mkimbizi:WFP

Apu ya simu kuwezesha mtu kuchangia mlo wake na mtoto mkimbizi:WFP

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limezindua leo apu ya simu ya mkononi inayowezesha mtu kuwalipia watoto wakimbizi wa Syria mlo wa shuleni.

Kupitia apu hiyo iitwayo “Share the meal” mtu yeyote anaweza kuamua kuchangia chakula chake na mtoto, kwa kutoa usaidizi wa senti 50 tu za kimarekani.

Akizungumza na Redio Ya Umoja wa Mataifa Sebastian Stricker, mkuu wa timu ya WFP iliyoandaa apu hiyo amesema idadi ya wamiliki wa simu za mkononi ni mara ishirini ya idadi ya watoto wanaokumbwa na njaa duniani na…

(sauti ya Bwana Stricker)

“ Tumegundua kwamba gharama ya kumlisha mtoto kwa siku moja ni senti 50 tu. Na tukafikiria kwamba iwapo kutakuwa na njia rahisi ya kutoa senti hizo 50, watu wengine wengi watatoa.”

Ameongeza kwamba Ujerumani, Austria na Uswisi ambako apu hiyo imefanyiwa majaribio tangu mwezi wa Juni, tayari milo milioni 1.7 imefadhiliwa barani Afrika, akisema:

(Sauti ya Bwana Stricker)

“ Tunaamini kwamba ubunifu unahitajika ili kuleta mabadiliko kwenye jamii na kuongeza kasi ya kufanya kazi ili kufikia dunia isiyokuwa na njaa.”

Mtu yeyote anayetaka kushiriki mradi huo anaweza kupakua apu hiyo Sharethemeal kwenda kwenye simu yake kutoka mifumo ya IOS na Android kuanzia tarehe 12 mwezi huu wa Novemba.