Mzozo wa Burundi ni wa kisiasa na hauwezi kumalizwa kijeshi- UM

Mzozo wa Burundi ni wa kisiasa na hauwezi kumalizwa kijeshi- UM

Mzozo uliopo nchini Burundi sasa ni wa kisiasa kimsingi, na hauwezi kutatuliwa kwa operesheni za vyombo vya usalama.

Hayo yamesemwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa, Jeffrey Feltman, wakati akilihutubia Baraza la Usalama ambalo limekutana kujadili hali nchini Burundi.

Bwana Feltman amesema kuwa mwelekeo unaotia wasiwasi, wa mauaji na mashambulizi kwa misingi ya kisiasa unapaswa kukomeshwa mara moja.

“Burundi inajikuta katika hali tete. Suluhu la kisiasa ni lazima lipatikane kuutanzua mzozo huu kabla uenee na kufikia kiwango kisichoweza kudhibitiwa, na kuathiri amani na usalama kikanda. Tunatumai kuwa wadau wa kimataifa, hususan wa kikanda, watazungumza kwa sauti moja, kwa kuisihi na kuisaidia Burundi kupata suluhu la kisiasa kwa mzozo huu.”

Aidha, Bwana Feltman ametoa ujumbe wa Katibu Mkuu..

“Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote za Burundi, ndani ya nchi na ng’ambo, kukomesha mara moja kueneza kauli za chuki, kujiepusha na ghasia na kushiriki kwa roho safi upatanishi unaoendelea wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Kadhalika, Feltman amesema Ban atatangaza karibuni kuteuliwa kwa mshauri maalum atakayeongoza na kuratibu juhudi za usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi.