Ban ataka ukatili na mauaji ya raia Burundi yakomeshwe

Ban ataka ukatili na mauaji ya raia Burundi yakomeshwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na kuendelea kuongezeka kwa ukatili nchini Burundi.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Ban akieleza hofu yake kuwa katika wiki chache zilizopita, kugundulika kwa miili ya wahanga ambao wengi wao wameuawa kiholela kumekuwa jambo la kawaida katika mitaa kadhaa ya Bujumbura.

Hofu hiyo ya Katibu Mkuu inafuatia mauaji ya mwanae Pierre-Claver Mbonimpa, mtetezi maarufu wa haki za binadamu nchini Burundi, baada ya kukamatwa na polisi mjini Bujumbura.

Ban amesema ukatili huo wa mara kwa mara na mauaji ni lazima vikomeshwe, huku akitilia msisitizo wajibu wa mamlaka za Burundi wa kuwalinda raia, bila kujali wanakoegemea kisiasa, pamoja na kuhakikisha kuwa ukwepaji sheria ulioshamiri kuhusu uhalifu huu unakomeshwa mara moja.

Aidha, Katibu Mkuu amelaani kauli zinazotolewa hadharani zikichochea ukatili au chuki dhidi ya makundi fulani nchini Burundi, akisema kuwa uchochezi kama huo utasababisha tu hali kuzorota zaidi nchini, na kutoa wito wawajibishwe wanaochochea ukatili na ghasia hadharani.