Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zaidi zaridhia kupunguza gesi chafuzi:UNEP

Nchi zaidi zaridhia kupunguza gesi chafuzi:UNEP

Kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabianchi mjini Paris, Ufaransa mwezi ujao, tangazo la kihistoria limetolewa linaloweka nuru katika kudhibiti utoaji wa gesi chafuzi na ufuatiliaji wa ongezeko la kiwango cha joto duniani.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP iliyotolewa leo ikizingatia kuwa nchi 150 tayari zimewasilisha mipango ya kudhibiti utoaji wa gesi hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Achim Steiner amesema karibu asilimia 90 ya uchafuzi wa hewa duniani unasababisha na mataifa na hivyo hatua hiyo ni ya kihistoria.

(Sauti ya Achim)

Nadhani tumeshuhudia kuelekea Paris, hatua za kihistoria na kusema kwamba kwa kuwa tayari tuna ahadi hizo ambazo unaweza kuelezea kama hatua za dunia kushughulikia changamoto ya ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi, tunaondoka kutoka pale tulipokuwepo mwaka mmoja au miwili iliyopita.”

Hata hivyo Steiner amehadharisha kuwa hata kama nchi hizo zitatekeleza mikakati hiyo, bado kiwango cha joto kitaongezeka kwa nyuzi joto Tatu mwishoni mwa karne hii kwa hivyo ni vyema  mazungumzo ya Paris yakaibuka na mkakati wa kudhibiti kiwango hicho.