Skip to main content

Kutoka MONUSCO, Kobler sasa ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Libya

Kutoka MONUSCO, Kobler sasa ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametangaza leo kuteuliwa kwa Martin Kobler wa Ujerumani kuwa Mwakilishi wake maalum na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL.

Bwana Kobler atamrithi Bernardino León wa Uhispania, ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa ari ya kazi yake na uongozi mzuri wa UNSMIL.

Bwana Kobler ana uzeofu wa zaidi ya miaka 30 ya kuhudumu kwenye ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa na katika huduma za kimataifa, akiwa amehudumu tangu mwaka 2013 kama Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO.

Kabla ya kwenda MONUSCO, Kobler aliwahi kuhudumu kama Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Afghanistan, UNAMA (2010-2011) na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Iraq, UNAMI kati ya (2011-2013).