Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO, Malawi wakabiliana na magonjwa yashambuliayo watoto

WHO, Malawi wakabiliana na magonjwa yashambuliayo watoto

Shirika la afya ulimwenguni WHO linafanya kazi na serikali ya Malawi kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya katika kutibu magonjwa ambayo hushambulia watoto kupitia mpango wa kupanua upatikanaji haraka (RAcE) unaofadhiliwa na serikali ya Canada ambao umezinduliwa mwaka 2013.

Katika mafunzo hayo mbinu itumikayo ni kujumuisha jamii katika kutatua magonjwa yanayoshambulia watoto (iCCM), msisistizo ukiwa kwa ugonjwa wa kuhara, malaria, vichomi vikali yaani pneumonia, ambayo kwa pamoja vilisababisha asilimia 45 ya vifo kwa watoto walioko chini ya umri wa miaka mitano nchini Malawi mwaka 2012.

Afisa wa uzuiaji wa mgonjwa katika wizara ya afya ya Malawi Dk Storn Kabuluzi amesema suala la kuzuia vifo ndilo lililosukuma uhitaji wa kuwa na mpango huo mwaka mmoja uliopita akisisitiza kuwa nchi hiyo iko mbioni kutimiza lengo hilo.

Mwaka 1990 kiwango cha vifo vya watoto walioko chini ya miaka mitano nchini Malawi kilikuwa vifo 245 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa. Mwaka 2013 idadi hiyo ilipungua hadi vifo 68 kwa watoto 1000 wanaozaliwa ikiwa ni punguzo la asilimia 72.