Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahofia watoto walioathiriwa na kimbunga Koppu, yahitaji dola milioni 2.8

UNICEF yahofia watoto walioathiriwa na kimbunga Koppu, yahitaji dola milioni 2.8

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limetangaza hali ya tahadhari kufuatia kimbunga Koppu (au Lando kwa jina la wenyeji) nchini Ufilipino mnamo Jumapili asubuhi.

Kimbunga hicho cha mwendo wa pole kilileta mvua nzito na upepo mkali, na hivyo kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi, kupotea umeme na kuvuruga mitandao ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa serikali, zaidi ya watu 55,000 wamehamishwa, na sasa zaidi ya familia 12,000 zinaishi katika vituo vya uhamisho wa dharura.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Ufilipino, Lotta Sylwander amesema kuwa cha kipaumbele kwa shirika hilo ni kuhakikisha kuwa watoto wako salama na wanalindwa, kwani wakati kama huu baada ya kimbunga, watoto hukumbwa na hatari kutokana na kuchafuliwa maji, kutokuwa na chakula, pamoja na magonjwa kama kipindupindu, kuhara na numonia.