Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera ya Ufilipino iliepusha hasara kubwa kufuatia kimbunga Koppu- UNISDR

Sera ya Ufilipino iliepusha hasara kubwa kufuatia kimbunga Koppu- UNISDR

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupunguza madhara ya majanga, UNISDR, Margareta Wahlström, leo ameipongeza Ufilipino kwa juhudi zake fanisi katika kupunguza wahanga na idadi ya watu walioathiriwa na kimbunga kilichoishambulia nchi hiyo hivi karibuni, licha ya mawimbi makubwa, mvua nzito, mafuriko na maporomoko ya ardhi.Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bi Wahlström amesema utoaji habari na tahadhari mapema nchini Ufilipino umeboreshwa sana tangu kimbunga Haiyan kuua watu 6,000 mwaka 2013, kufuatia sera ya serikali ya kulenga kuepusha vifo katika majanga ya vimbunga.

Amesema mwishoni mwa wiki iliyopita, mashirika ya serikali yalifanikiwa tena kupunguza idadi ya vifo kupitia utoaji habari upasao na tahadhari za awali, pamoja na kuandaa jitihada za kuwanusurisha watu katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na kimbunga Koppu. Mnamo Disemba mwaka jana, vifo vingi viliepushwa palipotokea kimbunga Hagupit.

Bi Wahlström amesema ingawa ukubwa wa hasara ya iliyosababishwa na kimbunga hicho haujajulikana bado, hapana shaka kuwa uhai wa watu wengi uliokolewa katika nchi hiyo ambayo ndiyo iliyoko katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na vimbunga duniani.