Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya watoto mizozoni inazidi kuzorota- Zerrougui

Hatma ya watoto mizozoni inazidi kuzorota- Zerrougui

Kumekuwa na ongezeko la kutoheshimu sheria ya kimataifa katika hali nyingi za mizozo duniani, na hivyo kuchangia kuzorota kwa hatma ya watoto, amesema Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na mizozo ya silaha, Zeila Zerrougui, akiwasilisha ripoti yake ya kila mwaka kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Bi Zerrougui amemulika nchi kadhaa ambako mizozo inaendelea, au hali tete na machafuko yanaongezeka, akisema kuwa watoto wanaathiriwa vibaya katika hali hizo.

Amesema Watoto ni takriban nusu ya idadi inayoongezeka ya wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makwao wakikimbia machafuko. Kila mwaka, nimekuwa nikisema hatma ya watoto katika mizozo imezorota. Kwa bahati mbaya, mwenendo huu haujabadilika.”

Ripoti hiyo ya kurasa 32 inamulika hali kati ya mwezi Agosti 2014 na Julai 2015, Bi Zerrougui akimulika pia vikundi vinavyoeneza vitendo vya ghasia na ukatili, akisema vimetenda uhalifu mbaya mno dhidi ya watoto.