Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bendera ya Palestina yapeperushwa UM

Bendera ya Palestina yapeperushwa UM

Leo ni siku ya kujivunia kwa wapalestina popote pale walipo duniani na ni siku ya matumaini.

Ndivyo alivyoanza hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati wa sherehe ya kupandisha bendera ya mamlaka ya Palestina kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, kufuatia azimio la Baraza Kuu mapema mwezi huu.

Ban amesema hatua ya leo ni ya kukumbusha watu kuwa alama ni muhimu na kwamba alama huelekeza katika mwelekeo sahihi.

Amesema kupandishwa kwa bendera hiyo ni ishara kwamba mamlaka ya Palestina imeazimia kusaka ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Palestina kuwa na taifa lao na azma ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono matamanio ya wananchi hao.

Amesema kufikia taifa lazima kuaminiana kati ya Palestina na Israel ili hatimaye kuwa na mataifa mawili yanayokuwepo pamoja.

Naye Rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft amesema siku ya leo inarejesha umakini wa kuimarisha haraka harakati za kusuluhisha mzozo kati ya pande mbili hizo ili hatimaye kuwa na taifa huru la Palestina linalokuwepo sambamba na taifa la Israel