Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon aiomba Ulaya ihurumie wakimbizi

Ban Ki-moon aiomba Ulaya ihurumie wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameziomba nchi za Ulaya kuwajibika na kuwapokea wakimbizi wanaotafuta hifadhi barani Ulaya bila kuwarudisha mpakani au kuwatesa.

Bwana Ban amesema hayo leo kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake akieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya mateso na ukiukaji wa haki unaokumba wakimbizi na wahamiaji wanaowasili Ulaya, akisisitiza kwamba tayari wamepitia hatari nyingi katika safari zao.

Taarifa hiyo inafuata ripoti za kufungwa kwa mipaka ya baadhi ya nchi za Ulaya na kufungwa kwa wasaka hifadhi na wahamiaji, pia ukosefu wa huduma za mapokezi.

Bwana Ban amewaomba viongozi wa Ulaya wahakikishe kwamba wakimbizi wanahudumiwa ipasavyo, na waonyeshe uongozi wenye huruma, wakati ambapo mkutano wa dharura wa Muungano wa Ulaya unatarajiwa kufanyika Jumatano hii.

Mkutano maalum kuhusu suala hilo unatarajiwa kufanyika pia tarehe 30 Septemba wakati wa mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.