Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Inasikitisha kambi za wakimbizi wa ndani zinaposhambuliwa: Beyani

Inasikitisha kambi za wakimbizi wa ndani zinaposhambuliwa: Beyani

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Chaloka Beyani, amelaani vikali shambulio la kikatili kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Yola, Kaskazini mwa Nigeria. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia.

(Taarifa ya Grace)

Kambi hiyo ni makazi ya wakimbizi 32,000 ambapo Beyani amesema shambulio hilo la kwanza tangu kuanza kwa mzozo kaskazini mwa nchi hiyo ni jambo la kusikitisha kwani ni eneo salama ambalo wao wanakimbilia.

Watu 14 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambuli hilo la tarehe 11 Septemba ambapo mtaalamu huyo amesema wakimbizi wa ndani ni watu walio hatarini zaidi na hivyo ni lazima walindwe dhidi ya mashambulio yoyote kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa.

Hakuna pande yoyote imekiri kuhusika na shambulio hilo lakini Bwana Beyani ametaka wasakwe na wafikishwe mbele ya sheria huku akitaka serikali iimarishe ulinzi kwenye kambi hizo.