Mtu mmoja kati ya wanne Afghanistan hana chakula: Ripoti

10 Septemba 2015

Ripoti mpya iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa na wadau wake imeeleza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini Afghanistan inazidi kuzorota.

Miongoni mwa viashiria vya kwamba hali ni mbaya, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni ongezeko la idadi ya watu wanaouza ardhi au kurejea kwa ndugu, jamaa na marafiki kusaka msaada kutokana na ukosefu wa chakula.

Ikipatiwa jina tathmini ya uhakika wa chakula Afghanistan mwaka 2015, ripoti imebaini kuwa katika msimu wa mwambo idadi ya watu wasiokuwa na uhakika wa chakula iliongezeka kutoka asilimia 4.7 mwaka mmoja uliopita hadi asilimia 5.9 hii leo.

Mwakilishi wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP nchini Afghanistan, Claude Jibidar amesema takwimu hizo zinatia wasiwasi hasa katika nchi ambayo theluthi moja ya wananchi wote tayari wana uhaba wa chakula.

Naye mwakilishi wa FAO Tomio Shichiri amesema ingawa Afghanistani inaweza kuzalisha ngano zaidi mwaka huu, bado hoja inayosalia siyo uzalishaji bali kukipata chakula na hivyo angalizo zaidi linatakiwa kwa kaya ambazo zinaongozwa na wanawake ili waweze kupata chakula, pamoja na wale watu wasio na makazi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter