Mkuu wa IAEA atoa ripoti kuhusu ajali ya Fukushima Daiichi

Mkuu wa IAEA atoa ripoti kuhusu ajali ya Fukushima Daiichi

Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, kuhusu ajali ya mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi, imetolewa leo, pamoja na nakala nyingine tano za kitaalum kuhusu suala hilo.

Ripoti hiyo iliyotolewa kabla ya kongamano la IAEA mnamo mwezi Septemba, inatathmini vyanzo na madhara ya ajali ya Machi 11 mwaka 2011 kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi nchini Japan, ambayo ilifuatia Tsunami na tetemeko kubwa la ardhi.

Ajali hiyo ndiyo iliyokuwa mbaya zaidi kwenye mtambo wa nyuklia tangu janga la Chernobyl la mwaka 1986.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukiya Amano, amesema ripoti hiyo inamulika masuala ya kibinadamu, kimfumo na kitaaluma, ikilenga kutoa uelewa wa kilichofanyika na kwa nini, ili mafunzo yatokanayo na tathmini hiyo yachukuliwe hatua na serikali, wadhibiti na wanaoendesha mitambo ya nishati ya nyuklia kote duniani.