Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara ya utumwa na marufuku yake yakumbukwa leo

Biashara ya utumwa na marufuku yake yakumbukwa leo

Leo ni Siku ya Kimataifa ya kukumbuka biashara ya utumwa na kupigwa kwake marufuku, maadhimisho ya mwaka huu yakiwa yanasadifiana na kuzinduliwa kwa Muongo wa Kimataifa wa Watu wenye Asili ya Afrika (2015-2024), ambao ulitangazwa mwaka 2014.

Katika kuadhimisha siku hii, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema kuwa kauli mbiu ya muongo huo, ‘Kutambua, Haki na Maendeleo’, inaona vyema na kazi na mradi wake wa Barabara ya Utumwa, ambo uliadhimisha miaka 20 mwaka uliopita.

UNESCO imesema siku hii ni ya kumulika ukubwa wa madhara ya janga hili la kibinadamu na utajiri wa utamaduni ulioenezwa na watu wenye asili ya Afrika wakati wakikabiliana na wakati mgumu, kupitia sanaa ya uchoraji, muziki, uchezaji ngoma, imani, fikra, hatua za kisiasa na upanuaji wa maarifa.

Maadhimisho hayo yanaonyesha pia kuwa utumwa sio tu kitu cha jadi, bali pia yanaonyesha jinsi biashara ya utumwa ilivyoathiri maumbile ya jamii ya sasa.