Sheria mpya ya kupinga utumwa Mauritania itekelezwe ipasavyo- Mtaalam wa UM
Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu aina za sasa za utumwa, Urmila Bhoola, amepongeza kupitishwa sheria mpya ya kupinga utumwa nchini Mauritania, ambayo imeongeza maradufu muda wa kufungwa wanaotenda uhalifu huo kutoka miaka 10 jela hadi 20, na kuweka jopo maalum la kushughulikia mashtaka ya kesi za utumwa. Taarifa kamili na Grace Kaneiya
(Taarifa ya Grace)
Hata hivyo, Bi Bhoola amesema, hatua hiyo nzuri inapaswa kufuatiwa na kutekelezwa ipasavyo, akiongeza kuwa utumwa na vitendo vinavyofanana na utumwa vinaweza tu kutokomezwa iwapo sheria na sera zilizopo zitatekelezwa kikamilifu na ipasavyo.
Mtaalam huyo maalum ameipongeza serikali ya Mauritania kwa kuchukua hatua muhimu ya kuibadilisha sheria ya mwaka 2007 dhidi ya utumwa, ambayo ilikuwa hafifu kwa upande wa kuwashtaki wahalifu.
Ameisifu sheria hiyo mpya iliyopitishwa na bunge la Mauritania wiki iliyopita, akisema kuwa inayapa haki mashirika ya kiraia kuwasilisha malalamishi kotini kwa niaba ya waathiriwa, ingawa baadhi ya vipengele vya sheria hiyo huenda vikazuia kufanya hivyo.