Ripoti ya UM yaonyesha ukwepaji sheria sugu Darfur
Uhalifu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika Darfur mnamo mwaka 2014, ukiwemo maujai na ukatili wa kingono, haujachunguzwa wala hawakuwajibishwa wakiukaji, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Ripoti hiyo iliyotokana na taarifa zilizotolewa na Ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika, AU na Umoja wa Mataifa Darfur, UNAMID, inabainisha visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na ukwepaji sheria ulioenea.
Kati ya visa 411 vya ukiukaji wa haki za kimwili uliotendwa na pande zote katika mzozo, ni vichache sana vilivyochunguzwa au washukiwa kukamatwa. Visa 127 kati ya visa vyote 411 vilihusu ukatili wa kingono.
Ofisi ya Haki za Binadamu imesema idadi hii inaashiria mwenendo ulioenea wa ukatili.