Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya #ShareHumanity yazinduliwa kuadhimisha Siku ya Kibinadamu

Kampeni ya #ShareHumanity yazinduliwa kuadhimisha Siku ya Kibinadamu

Umoja wa Mataifa na wadau wake, leo wamezindua kampeni ya kidijitali ya kuhadithia kuhusu ubinadamu iitwayo #ShareHumanity, siku chache kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kibinadamu Duniani, Agosti 19.

Kupitia kampeni hiyo, watu kote duniani watatumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kueneza hadithi za wale walioathiriwa na mizozo ya kibinadamu katika nchi kama vile Syria, Sudan Kusini na Afghanistan.

Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi leo kwa ushirikiano wa mwimbaji wa Australia, Cody Simpson, mwanakarata wa Kichina, Jet Li na Muingereza mkwasi, Richard Branson na mwanasoka wa Brazil, Kaká.

Siku ya Kibinadamu Duniani iliwekwa na Baraza Kuu mnamo mwaka 2008, katika kuadhimisha shambulizi la bomu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad, ambalo liliwaua watu 22.