Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahimiza subira na utulivu baada ya Ebola kushukiwa Tanzania

UM wahimiza subira na utulivu baada ya Ebola kushukiwa Tanzania

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na Shirika la Afya Duniani, WHO, yametoa wito wa utulivu kufuatia ripoti za kifo cha mkimbizi wa Burundi kinachoshukiwa kutokana na kirusi cha Ebola, mnamo Agosti 10 2015. Taarifa ya Priscilla

(Taarifa ya Priscilla)

Mkimbizi huyo ambaye alikuwa ameishi katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu kwa muda wa miaka mitatu akisubiri kuhamishiwa Marekani, alifariki dunia katika hospitali ya Maweni katika mkoa wa Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Mnamo Agosti 9, mkimbizi huyo alipelekwa kwa hospitali ya Maweni, akiwa anatokwa damu katika ufizi, macho na masikio. Alikuwa pia amechoka, huku mwili ukiwasha, ingawa hakuwa na homa.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez ameiambia idhaa hii kwamba uwezekano kuwa ni Ebola ni mdogo, hata hivyo Tanzania imejitayarisha kukabiliano na mlipuko wa aina hiyo.

(Sauti ya Alvaro Rodriguez)

"Kuna mpango wa kitaifa wa kudhibiti Ebola, pamoja na mpango wa dharura wa Umoja wa Mataifa, kwa hiyo kuna kiwango fulani cha kujiandaa. Hatuamini kwamba ni kisa cha Ebola, lakini iwapo kisa cha Ebola kitaibuka, tunaamini kwamba misingi ya kazi imewekwa. Hata hivyo, kama Afrika Magharibi, itakuwa changamoto kubwa kwa nchi yenye idadi kubwa ya watu kukabiliana na ugonjwa huo. »

Taarifa ya pamoja ya WHO na UNHCR imesema hakuna ushahidi wowote kuwa mtu huyo alikuwa amesafiri nje ya mkoa wa Kigoma au kupokea wageni kutoka nchi zilizoathiriwa na Ebola Afrika Magharibi. Mashirika hayo yamesema vipimo vya awali pia havijaonyesha dalili za Ebola, na hivyo shughuli za kila siku zisivurugwe. Vipimo vingine vinafanywa kubaini ugonjwa uliomuua mkimbizi huyo.

.