Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwango vya juu vya usafi vimezuia Ebola kusamba shuleni: UNICEF

Viwango vya juu vya usafi vimezuia Ebola kusamba shuleni: UNICEF

Wakati ambapo wanafunzi wa Guinea, Sierra Leone na Liberia wanaanza likizo yao ndefu ya msimu wa joto, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema hatua zilizochukuliwa kuzuia maambukizi zimewalinda dhidi ya mlipuko wa Ebola.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imekaribisha mafanikio hayo, ikieleza kwamba watoto wamejifunza kujitunza na maambukizi ya Ebola na wameweza pia kuhamasisha wazazi wao na jamii zao, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kutokomeza ugonjwa huo.

Aidha UNICEF imeeleza kwamba hakukuwa na kisa kimoja cha Ebola shuleni  kwenye nchi hizo tatu baada ya shule kuanza upya mwanzo mwa mwaka huu.

Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kupima halijoto ya wanafunzi na walimu, na kujenga sehemu maalum za kunawa mikono, pamoja na kusambaza mamilioni ya miche ya sabuni, na kufundisha makumi ya maelfu ya walimu.

Hata hivyo, changamoto bado zipo, UNICEF ikitaja kiwango kidogo cha uandikishaji wa watoto shuleni na upatikanaji wa huduma za maji safi.